Thursday, August 30, 2012

JENGO LENYE KABURI LA BABA WA TAIFA ENEO LA MWITONGO BUTIAMA

Makamu wa CCM Tanzania Bara mzee Pius Msekwa mwenye shati la kijani katika akiwa na mwenyekiti wa ccm mkoa Mara Bw Cherles Makongoro Nyerere na viongozi wengine wa kijiji cha Butiama wakitoka ndani ya banda lilimo kaburi la Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius K Nyerere,kutoa heshima wakati mzee msekwa alipotembelea familia ya baba wa taifa kijiji hapo.

 
Na George Marato,Musoma

VITA ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2015,imetajwa kuwa chanzo cha kuhakikisha lazima Makongoro Nyerere ang’olewe katika kutetea nafasi yake uenyekiti wa CCM mkoa wa Mara kwenye uchaguzi unaotarajia kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu.

Makongoro ambaye ni mtoto wa tano wa Baba wa taifa hayati mwalimu Julius Nyerere,amekuwa mwenyekiti wa ccm mkoa wa Mara kwa miaka mitano inayomalizika sasa,amethibitisha kuwapo kwa njama hizo ambazo amedai zinatokana na msimamo wake wa kutaka chama kuwafukuza viongozi ambao kwa namna moja ama nyingine wamekuwa wakituhumiwa kwa ufisadi na kusababisha kushusha heshima ya chama hicho mbele ya jamii.

Alisema kutokana na msimamo huo, kuna baadhi ya watu wanaominika kumuunga mkono mmoja ya watu wanaotajwa kugombea nafasi ya urais mwaka 2015 kupitia chama hicho na wenye uwezo mkubwa kifedha wakiwa nje na ndani ccm mkoani Mara,wamepanga kununua kila kura ya mjumbe mmoja wa mkutano mkuu kwa shilingi laki moja hadi laki moja na nusu ili kuhakikisha mwanasiasa huyo anang’oka katika nafasi hiyo.

“Ni kweli nimepata taarifa kuna fungu kubwa limepangwa ili kuhakikisha linaning’oa ndio maana wamemfuta mmoja ya watu ambao historia inaonyesha miaka yote walikuwa hawaivi lakini sasa wamemshawishi kuchukua fomu na kumchangia fedha ili kufanikisha mkakati wao…lakini mimi sina wasiwasi hata kidogo nimechukua fomu naijaza na kurejesha kwani najua wenye uamuzi wa mwisho ni wajumbe wa mkutano mkuu sio fedha zao”alisema Makongoro kwa njia ya simu endapo anatetea nafasi yake hiyo.


Inadaiwa kuwa chuki kubwa za kuhakikisha Makongoro anang’olewa katika nafasi hiyo hata bila kujali gharama zitakazotumika nikutokana na msimamo wake katika kukiongoza chama hicho bila kuhitaji kundi pili kukataa kwake kupanda majukwaani mwaka 2010 katika uchaguzi mkuu ili aweze kumtukana mdogo wake Vicent Nyerere aliyekuwa anagombea ubunge kupitia Chadema.

Kwa mujibu wa habari kutoka ndani ya ccm Musoma mjini na kutoka kwa baadhi ya viongozi wa mkoa,walimshinikiza Makongoro kutumia ukaribu wake na mgombea huyo wa Chadema kupanda katika majukwaa na kumshambulia hata kumkana kuwa si ndugu yake kama mkakati ambao ungesaidia ccm kushinda katika jimbo la Musoma mjini, jambo ambalo lilipingwa vikali na Makongoro kwa madai hawezi kumtolea lugha ya matusi mdogo wake kwa misingi tu ya siasa.


Kutokana na msimamo huo wa Makongoro ulimfanya kuchukiwa na baadhi ya viongozi wa ccm wa mkoa tena wenye ushawishi mkubwa kifedha na wale wa Musoma mjini hivyo kuanza mikakati mbalimbali ya kumng’oa kupitia katika vikao lakini walishindwa,pia wakajitokeza kumchafua wakati akigombea ubunge wa afrika mashariki mkakati ambao pia ulishindwa na hivi sasa nguvu kubwa imeelekezwa katika uchaguzi huo.

Hadi jana tayari wanachama watatu wa ccm,wamechukua fomu za kugombea nafasi ya uenyekiti wa ccm mkoa wa Mara pamoja na Makongoro,pia wamo Dommy Athumani Juma na aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho miaka kumi iliyopita Enock Mwita Chambiri kabla ya kutangaza kustafu nafasi hiyo katika uchaguzi mkuu wa chama hicho mwaka 2007.

Chambiri alitangaza kustafu uenyekiti mwaka 2007 katika mkutano mkuu wa uchaguzi wa chama hicho,ambao ulimwingiza Makongoro madarakani kwa kusoma alama za nyakati wakati huo kutokana na makundi yalikuwepo na kumpinga huku akisema anaiachia nafasi hiyo lakini atasita kurudi tena endapo ataona chama hicho kinayumba.

Vita ya Makongoro pia imeelezwa inaweza kumkumba mbunge wa Musoma vijijini Nimrod Mkono ambaye tayari amechukua fomu za kugombea uenyekiti wa wazazi taifa baada ya kutuhumiwa kuwa ndiye aliyemsadia Makongoro Nyerere kushinda vita ubunge wa afrika mashariki.

Wakati huo huo kasi ya wanachama wa CCM kuchukua fomu za kuwania nafasi mbalimbali
za uongozi ndani ya chama hicho mkoani Mara inazidi kuongezeka hasa katika nafasi za ujumbe wa halmashauri kuu kupitia wilaya.

Miongoni mwa vigogo walichukua fomu hizo ni mfanyabiashara maarufu Christopher Gachuma(Tarime),Thobias Raya(Rorya) Marwa Siagi(Musoma vijijini),Vedastus Mathayo (Musoma mjini) akiwemo mwandishi mwandamizi wa habari Cyprian Musiba
kujitosa kuomba nafasi hiyo katika wilaya ya Bunda.

Mchuano katika nafasi za halmashauri kuu taifa kupitia ngazi ya wilaya unatarajia kuwa mkali zaidi kutokana na idadi kubwa ya wanachama kujitokeza kuchukua fomu hizo.

No comments:

Post a Comment