Na George
Marato,Musoma
Kufuatia
mauji ya kinyama na kutisha kuibuka mkoani Mara,hatimaye jeshi la Polisi mkoani
humo,limetoa tahadhari kubwa kwa wananchi wa Mkoa huo hasa Wanawake wa maeneo ya vijijini kuwa makini wakati wakiwa katika shughuli kilimo na
utafutaji wa kuni.
Pamoja na
tahadhari hiyo pia wananchi hasa wanawake wameombwa kutoa taarifa polisi pindi
tu wanaposhuku kuwepo kwa jambo lolote ambalo linahatarisha maisha yao ili
hatua za haraka ziweze kuchukuliwa.
Kaimu
kamanda wa polisi mkoa wa Mara SSP Japhet Lusingu,ametoa taadhari hiyo jana
ofisi kwake mjini hapa wakati akiongea na waandishi wa habari kuhusiana na
matukio ya mauji ambayo yameibuka katika siku za hivi karibuni mkoani Mara hasa
katika wilaya ya Butiama na Manispaa ya Musoma .
Alisema
tayari jeshi la polisi linawashikiria watu sita kuhusiana na mauji ya Sabina
Mkireri mkazi wa kijiji cha Kiemba ambaye aliuawa kwa kuchinjwa kisha wauji
kuondoka na kichwa chake Desemba tatu mwaka huu.
“Nachukua
nafasi hii kuwatoa hofu wananchi kuhusu mauji haya,lakini natoa taadhari kwa
wakina mama hasa wa maeneo ya vijijini wanapokuwa katika shughuli za kilimo na
utafutaji wa kuni wawe waangalifu na watoe taarifa mapema pindi tu wanaposhuku
kuwapo kwa jambo lolote lisilo la kawaida”alisema kaimu kamanda huyo ambaye pia
ni afisa mnadhimu wa jeshi la polisi mkoa wa Mara.
Aidha
alisema Desemba mbili mwaka huu majira ya saa moja usiku Brandina Peru alikutwa
polini akiwa amekufa baada ya kuchinjwa.
Kaimu
kamanda huyo wa polisi mkoa wa Mara,alisema marehemu kabla ya kuuawa kikatili
aliondoka nyumbani kwake desemba mosi mwaka huu akiwa peke yake kwenda porini
kukata kuni na hakuweza kurudi nyumbani hadi alipokutwa amekufa kwa kuchinjwa.
Hata hivyo
alisema kabla ya kuchinjwa wauaji hao walimvua nguo zote na kuweka kando kisha
kumbaka na kwamba hakuna mtu yoyote aliyekamatwa hadi sasa na chanzo cha tukio
bado kinachunguzwa.
Kwa sababu
hiyo alisema jeshi la polisi limejipanga kikamilifu kwaajili ya kuwasaka watu
wanahusika na vitendo hivyo huku akiwaamba waandishi wa habari na viongozi wa
kisiasa kutowatia hofu wananchi kwa kutoa taarifa bila kuthibitishwa na vyombo
vya dola.
Kuhusu
taarifa za viungo hivyo vya binadamu kutumika kwa imani potofu kwa shughuli za
uchimbaji wa madini na uvuvi wa samaki alisema jeshi hilo linachunguza ukweli
wa taarifa hizo.
Wakati huo
huo,kamanda Lusingu,alisema mwanafunzi mmoja Hamis Lazaro wa kidato cha pili
katika shule ya sekondari ya Etaro ameuawa kwa kushambuliwa,mawe na
kukatwakatwa na mapanga katika sehemu mbalimbali za mwili wake.
Alisema
tukio hilo lilitokea saa 11.30 katika kijiji cha Kwikerege kata ya Etaro wilaya
Butiama baada ya kukutwa chini ya uvungu wa kitanda kilichokuwa kikitumiwa na
Nyakongo Nyangata ambaye alikuwa na mahusiano ya kimapenzi.
Hata hivyo
kamanda huyo alisema mbali na madai ya marehemu kuwa na mahusiano ya kimapenzi
na mwanafunzi huyo mwenzake lakini wananchi walijichukulia sheria mkononi baada
ya kuisi kuwa ni miongoni mwa watu ambao wamekuwa wakishiriki katika vitendo
vya mauji ya kinyama katika eneo hilo.
Mwisho
Na George
Marato,Musoma
SAKATA la
mauji ya kinyama mkoani Mara,imani za kishirikina ni moja ya sababu kubwa
ambazo zimetajwa kuwa chanzo kikuu cha mauji hayo ambayo yameibuka kwa kasi kubwa katika mkoa huu hasa kwa wilaya za Butiama
na Musoma mjini huku wauaji wakichukua baadhi ya viungo vya binadamu kwa madai
ya kusadia shughuli za uvuvi wa samaki na uchimbaji wa dhahabu.
Imedaiwa
kuwa wauji hao wengi wamekuwa wakitoka mkoa wa Kigoma wakiwa ni wenyeji wa nchi
jirani ya Congo ambao wamekuwa wakishirikiana na wenyeji katika maeneo hayo
kisha kufanya mipango ya mauji hayo ya kinyama.
Baadhi ya
wavuvi na wachimbaji wadogo wa madini,wamedai kuwa wauji hao wamekuwa wakiuza
vichwa vya watu kwa imani za kishirikina kwaajili ya shughuli za uchimbaji wa
dhahabu huku ndimi,matiti na sehemu za siri vikitumika kwaajili ya uvuvi katika
ziwa Victoria.
Aidha
imedaiwa kuwa baadhi ya Mangariba pia kutoka eneo la Tarime na Kiagata wamekuwa
wakiwauzia wavuvi viungo vya mwanamke baada ya kuwakeketa jambo ambalo
limetajwa kuwa chazo cha kusababisha wimbi la mauji ya watoto wa kike ambao
wamekuwa wakiuawa kisha kunyofolewa viungo hivyo yakiwemo na matiti.
Hata hivyo
baadhi ya wavuvi ambao wameomba kuhifadhiwa majina yao kutoka visiwa ndani ya
ziwa victoria wakizungumza kwa njia ya simu na Nipashe Jumapili kwa nyakati
tofauti,wamedai kuwa pamoja na matajiri wao kununua viungo hivyo kutoka kwa
baadhi ya watu lakini hakuna mabadiliko yoyote ambayo wamekuwa wakiyapata.
“Kweli kuna
wakati watu wanakuja eti ni waganga kisha wanakwenda ziwani usiku na matajiri
na mwakilishi wa wavuvi kwa kila mtumbwi ili
kuonyesha nyavu zilipo wakifika wanachukua vitu kama nyama wanasugua
kila mwesho wa nyavu lakini hatujawahi kuona mabadiliko ya kuongeza
samaki”alisema mmoja ya wavuvi.
Wavuvi hao
waliongeza kuwa watu hao wanaoisi kuwa ni waganga wamekuwa wakiwazuia kuongea
kitu chochote wakati wa zoezi la kufanya mitambiko hiyo huku wao wakizungumza
lugha na maneno wasio yaelewa hadi zoezi hilo linapo malizika.
Walipohojiwa
ni kwanini wanashindwa kutoa taarifa hizo kwa vyombo vya dola wavuvi hao
walidai kuwa wanashindwa kufanya hivyo kwa kuhofia maisha yao kwa vile wamiliki
wengi wa zana hizo za uvuvi wana mahusiano makubwa na baadhi ya maafisa ambao
wako katika vyombo vya dola.
Hata hivyo
wachimbaji hao wa dhahabu wameshindwa kuwa wazi kila walipoulizwa ili
kuthibitisha viungo hasa vichwa vya binadam vimekuwa vikitumika wakati gani na
kwa maeneo yapi.
Kwa upande
wake mbunge wa Musoma vijijini Nimrod Mkono,pamoja na kutoa pole kwa wote ambao
wamekumbwa na janga hilo,lakini alisema jeshi la polisi linapaswa kuwachunguza
wanasiasa kwani alisema wakati mwingine wamekuwa wakishiriki katika ushirikina
huo kwaajili ya kujipatia fedha.
“Hali hii
inatisha inawezekana vitu hivi vikatumika kwa ushirikina katika madini na uvuvi
lakini miongoni mwetu wanasiasa ni vyema tukachunguzwa kwani wengini
hawamuogopi mungu wanaweza kufanya mchezo huo mchafu kwaajili ya kupatafuta
pesa za uchaguzi na wengine kufanyia mitambiko ya biashara zao”alisema Mkono
kwa njia ya simu na kuongeza
“Hilo ni
jambo kubwa haiwezekani mtu wa kawaida tu akaenda kumchinja mtu na kuondoka na
kichwa chake bila ya kuwapo kwa mkono wa watu wenye uwezo,hivyo ni vyema jeshi
la polisi likafanya uchunguzi wa kina kuhusu hali hii”alisema.
Juzi mbunge Musoma
mjini Vicent Nyerere(Chadema) alimtaka mkuu wa jeshi la polisi nchini (IGP)Said
Mwema kuchukua hatua sasa kuhusu mauji mauji ya kikatili ambavyo yameibuka
katika Manispaa ya Musoma na wilaya ya Butiama.
Akizungumza na
gazeti hili kwa njia ya simu alisema katika kipindi cha mwezi mmoja tu zaidi ya
watu kumi na saba wameuawa huku wengine wakichinjwa kicha waujia kuondoka na
vichwa na viungo vyao vingine vya miili yao.
Alisema
pamoja na hali hiyo ambayo imechangia hofu kubwa kwa wananchi lakini hakuna
jitihada zozote zinazochukuwa kwaajili ya kukabiliana na vitendo hivyo vya
kinyama.
Aidha mbunge
huyo alimtaka pia Rais Jakaya Kikwete kuchukua hatua kwa wenyeviti wa kamati za
ulinzi na usalama wa wilaya hizo ambao amedai baadhi yao wameshindwa kusimamia
majukumu yao na kubaki kuendesha siasa wakati wananchi wakizidi kuawa kinyama
na wengine kuachwa na vilema vya maisha.
“Ni tatizo
kubwa ndani ya mwezi mmoja tu watu kumi na saba wameuawa kinyama na wengine
kuchinjwa lakini mbali na vyombo vya dola kukaa kimya hata nyinyi waandishi
mmeshindwa kujulisha umma kuhusu ukatili huu”alisema Nyerere na kuongeza.
“Rais mtoe
mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wilaya(DC) hapo Musoma amekalia siasa
na kuacha majukumui ya serikali katika kulinda raia na mali zao hii ni hatari
kubwa”aliongeza.
Hata hivyo
wakati mbunge huyo akitoa kauli hiyo,mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama
wa wilaya ya Butiama Angelina Mabula,ameliagiza jeshi la polisi kufanya kazi
usiku na mchana katika kuhakikisha linawatia mbaloni watu wote ambao wanahusika
na mauji ya kikatili ya raia.
Mabula
ambaye ni mkuu wa wilaya ya Butiama,alitoa agizo hilo juzi jioni baada ya
kuokotwa kwa mama mmoja Sabina Mkereri (46)ambaye alichinjwa na wauji kuondoka
na kichwa chake katika kijiji cha Kabegi kata kata ya Nyakatende.
“Nawaomba
wananchi mtoe ushirikiano wa kutosha ili kuhakikisha wahusika wote wanasakwa na
kuanzia sasa naagiza kuanza kwa vikundi vya ulinzi shirikishi kwaajili ya
kufanya kazi ya kuwasaka watu hawa usiku na mchana…jamani tunaipeleka wapi
Tanzania yetu yenye amani kwa kufanya matendo haya ya kinyama”alisema DC
Mabula.
Kaimu
kamanda wa polisi mkoa wa Mara SSP Japhet Lusingu,akizungumza na gazeti hili
pamoja na kukiri baadhi ya watu kuchinjwa na viungo vyao kuchukuliwa lakini
alisema idadi inayotajwa si sahihi.
Alisema
tayari jeshi la polisi limechukua hatua mbalimbali za kukabiliana na vitendo
hivyo vya kinyama huku akisema jeshi lake linachunguza kuhusu viungo hivyo
kutumika kwa shughuli za uvuvi na ushirikiana.
Hata hivyo
aliwaomba waandishi na viongozi wa siasa kuacha kutoa taarifa ambazo si sahihi
bila kuthibitishwa na jeshi hilo ili kutowaweka katika hali ya hofu wananchi.
Mwisho
No comments:
Post a Comment