Friday, September 7, 2012

HABARI NA MATUKIO MBALIMBALI KATIKA UZINDUZI WA MRADI WA KUWAJENGEA UWEZO WANAWAKE CHINI YA KANISA LA ANGLIKANA WILAYANI BUNDA MKOANI MARA


RUSHWA imetajwa ni kikwazo kikubwa kwa wahisani kusadia miradi nchini

Na George Marato,Bunda

SERIKALI wilayani Bunda mkoani Mara,imekiri kuwa vitendo vya Rushwa hasa katika Taasisi za serikali nchini,vimekuwa ni kikwazo kikubwa ambacho kimefanya hata wahisani kusita kuisadia serikali katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

Kauli hiyo imetolewa wilayani hapa juzi na mkuu wa wilaya ya hiyo Joshua Chacha Mirumbe,wakati wa uzinduzi wa mradi wa kuwajengea Uwezo Wanawake wa vijiji sita katika wilaya ya Bunda na Butiama kupitia kanisa la Anglikan Doyosisi ya Mara chini ya Ufadhili wa shirika la TEAR la nchini Australia.

Alisema mbali na taasisi za serikali pia mashirika yasiyakuwa ya kiserikali yamekuwa yakitumia vubaya fedha za wahisani kwa kushindwa kuwafikia walendwa kama walivyokusudia hatua ambayo pia imechangia kuwavunja moyo wafadhili.

Kwa sababu hiyo,amewataka viongozi wa dini pamoja na kuwahudumia wananchi kiroho lakini pia watambue wana jukumu la kuhakikisha wanaijenga jamii yenye maadili mema katika kuhakikisha taifa linaondokana na vitendo vya rushwa na imani kwa wafadhili.

“Kikwazo kikubwa nchini kwetu kinachochangia kurudisha nyuma maendeleo ni tatizo la rushwa,tatizo hili limefanya hata wahisani wetu kusita kutusadia sasa baba askofu pamoja na kuilea jamii kiroho pia mnajukumu la kuhakikisha mnailea jamii katika maadili mema ili iweze kuondokana na tatizo la rushwa katika kurejesha imani kwa wahisani wetu”alisema na kuongeza.

“Kwa kweli nalipongeza kanisa la Anglikana kwa kuleta mradi huu katika vijiji vinne vya wilaya yangu na viwili katika wilaya ya Butiama,mimi nawapongeza kwani mmeilenga jamii husika kwa vile utafiti umeonyesha wilaya hizi mbili ni miongoni mwa wilaya tano za mwisho kwa umasikini na kuliwezesha kundi hili la wanawake umesaidia jamii nzima”alisema.

Hata hivyo kiongozi huyo wa wilaya ya Bunda,alitumia nafasi hiyo kuwaagiza wananchi na viongozi katika vijiji unapotekelezwa mradi huo,kutoa ushirikiano wa dhati kwaajili ya kurejesha imani kwa wafadhili wa ndani na nje ya nchi katika kusadia miradi ya maendeleo na ile ya kiuchumi na hivyo kuzindoa wilaya hiyo kuwa ya mwisho kwa umasikini nchini.

Mkuu huyo wa wilaya ya Bunda ametumia nafasi hiyo kuwaagiza viongozi wenyeviti na watendaji wa vijiji vyote vya wilaya hiyo, kuandaa mipango maalum ya kilimo kwa kuanda madaftari ya kuorodhesha mashamba ya kila kaya katika kuhakikisha wilaya hiyo sasa inaondokana na tazizo la njaa linalojitokeza mara kwa mara.

Alisema tayari viongozi hao wa vijiji,wameagizwa kuandaa madaftari hayo ambayo yatatumika kuorodhesha mashamba ya mazao ya chakula na biashara kwa kila kaya kuanzia sasa.

Alisema kuwa kamwe serikali haitasita kuwakamata na kuwafungulia mashitaka viongozi hao wa vijiji watakashindwa kutekeleza agizo hilo na kuweka mipango  mizuri ya kufanikisha kilimo ambacho pia kinalenga kuinua uchumi wa wananchi.

“Tunamaliza Sensa nimewaambia viongozi wote wa vijiji kuelekeza nguvu zao katika kilimo kwa kuhakikisha kila kaya inalima mazao ya biashara na chakula nikija kufanya ukaguzi na kukuta hamjatekeleza maagizo haya nitaanza kuwashughulikia sasa si wakati wa kufanya siasa ni wakati wa kufanya maendeleo”alisema Mirumbe.

Hata hivyo mkuu huyo wa wilaya ya Bunda, alisema serikali wilayani hapa imeanzisha utaratibu wa kupima utendaji wa kila kiongozi wa kijiji kwa jinsi anavyojishughulisha na utatuzi wa kero zinazowakabili wananchi katika eneo lake  pamoja na kutanguliza mbele utawala wa  bora unazingatia sheria na kwamba atakaeshindwa kufanya hivyo ni vyema akajiondoa mwenyewe katika nafasi hiyo.

Akitoa taarifa kwa mkuu huyo wa wilaya,mratibu wa mradi kutoka kanisa la Anglikan Dr Theophil Kayombo,alisema mradi huo unatarajia kugharimu kiasi cha shilingi milioni 350 na kuwafikia wanawake 240 walioko kwenye vikundi mbalimbali.

Alisema licha ya wanawake hao pia wanajamii zaidi elfu kumi kupitia mikutano ya hadhara na mafunzo mbalimbali katika vijiji vya Tairo,Karukekere,Kitaramanka na Serengeti wilayani Bunda huku wilaya ya Butiama vijiji vitakavyonufaika ni Masinono na Bugwema.

“Mradi huu wa miaka mitatu umetokana na tafiti zilizofanywa na wadau mbalimbali wa maendeleo ambazo zinaonyesha kuwa wanawake wamekuwa wakitoa mchango mkubwa sana katika shughuli za maendeleo lakini jamii haijathamini mchango wao kutokana na mfumo dume uliopo pia ushirikishwaji mdogo wa wanawake katika maamuzi kwa ngazi mbalimbali”alisema Dr Kayombo.

Kwa upande wake baba askofu wa kanisa la anglikana dayosisi ya Mara, Mhashamu Hilkia Omindo Deya, amewaomba viongozi wa vijiji kutoa ushirikiano wa kutosha kwa mkuu huyo wa wilaya ili kuwezesha wilaya hiyo kupiga hatua kimaendeleo na kiuchumi.


Wakati huo huo kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya ya Bunda,imesitisha kwa muda malipo ya jumla ya shilingi  bilioni 1.2 ambazo zilikuwa zilipwe kwa wananchi wa kitongoji cha Kirumi wanaotakiwa kupisha eneo hilo kwa ajili ya shughuli za uwekezaji za EPZA.

Hatua hiyo inafuatia baada ya kubaika kuwa kuna idadi kubwa ya majina hewa ya watu kutoka maeneo mbalimbali pamoja na nje ya wilaya hiyo ambayo yameorodheshwa kwaajili ya malipo hayo wakati si wakazi wa eneo hilo.

Mwenyakiti wa kamati hiyo ambaye pia ni mkuu wa wilaya Bunda Joshua Mirumbe, amesema kuwa serikali hivi karibuni imeleta kiasi cha shilingi bilioni 1.2 kwa ajili ya kuwalipa wananchi ambao wanatakiwa kuhama eneo hilo lakini imegundulika kuwa kuna mchezo mchafu ambao ulikuwa umeshaandaliwa na baadhi ya wajanja katika halimashauri hiyo ili waweze kuhujumu malipo hayo.


Alisema kuwa wakati pesa hizo zikiletwa kulikuwa na zoezi la sensa ya watu na makazi na pia wilaya ilikuwa ina maandalizi ya kupokea Mwenge wa Uhuru hivyo kamati ya ulinzi na usalama haikuweza kupata nafasi ya kuhakiki majina ya watu wanaostahili kulipwa kama kweli ni wenyewe ama jambo lilotoa mwanya kwa wajanja kuingiza majina hayo hewa.

Kwa sababu hiyo alisesema kuwa wakati bado kamati ya ulinzi na usalama inajipanga ameshangaa kuona halmashauri ya wilaya ikianza kuwalipa wananchi wa kitongoji hicho pasipo mpangilio jambo alilosema kuwa lingeweza kuleta manung’uniko makubwa kwa wananchi wengine ambao ndio wakazi wa eneo hilo.


Amefafanua kuwa baada ya ofisi yake kupata taarifa ya kuwepo kwa majina hewa tayari ameunda tume ya kuhakiki majina hayo na kwamba kazi hiyo inaendelea vizuri na pindi itakapokamilika wale wanaostahili kulipwa watalipwa haki zao.

Hata hivyo aliwataka wale wote watakaokuwa wamelipwa pesa zao wahakikishe wanahama na kuachia eneo hilo na watafute maeneo mengine ya kuishi  ili liweze kuanza kufanyiwa maandalizi ya uwekezaji huo wa EPZ.

Mwisho

No comments:

Post a Comment